Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mwandishi wa makala hiyo ameeleza kushangazwa na jinsi Wamyanmari wanaoandamana sasa walivyonyamazia kimya mauaji ya kimbari na ukatili unaoendelea kufanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ikiwa ni pamoja na kuchoma moto vijiji na makazi yao, kunajisiwa wanawake na mabinti zao na hatimaye kuwalazimisha malaki miongoni mwao kuwa wakimbizi katika nchi mbalimbali hususan Bangladesh.
Hata hivyo mwandishi wa The Observer amepongeza maandamano ya sasa nchini Myanmar akiyataja kuwa ni ya kishujaa licha ya kuwalaumu waandaaji wa maandamano hayo kuwa wamefumbia jicho maafa yanayowakuta Waislamu wa Rohingya ambao aghlabu yao wanaishi katika jimbo la Rakhine Kaskazini Magharibi mwa Myanmar.
Gazeti la The Observer limeandika kuwa, Baraza la Kijeshi la Myanmar lililotwaa madaraka ya nchi mwaka 1962 lilieneza chuki dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya kama wenzo wa kuimarisha nafasi yake baina ya wanachi na likaanza operesheni ya mauaji ya kimbari ambayo yalishadidi zaidi mwaka 2017 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Mwandishi wa makala hiyo amesema kwa sasa kuna tetesi za kuwepo mawasiliano baina ya harakati ya kutetea demokrasia nchini Myanmar na vinara wa Waislamu wa Rohingya na kwamba baadhi ya Waislamu hao wamejiunga na maandamano yanayopinga mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
Itakumbukwa kuwa jana mamilioni ya Wamyanmari walianza mgomo wa nchi nzima wa kupinga hatua ya jeshi ya kutwaa madaraka ya nchi.
Tarehe Mosi ya mwezi huu wa Februari jeshi la Myanmar lilitangaza kudhibiti madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi nchini Myanmar, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo ambayo ilizua hofu ya kutokea mapinduzi.
342/